A.Y
AY anakuwa news siku ya leo huku akilalamika kuwa wasanii wa kibongo wamelala mnoo na kama wakiendelea hivyo hawataambulia chochote zaidi ya kubaki kulalamika kila kukicha.
Msela huyu anayefanya vyema kunako sanaa hapa Afrika Mashariki anasema wasanii wengi wa humu nchini wamezubaa na hawana uchu wa maendeleo ya kutaka kujua kinachoendelea sayari nyingine.
"Ukiangalia hali ilivyo utaona kabisa watu hawana uchu wa maendeleo, wapo wapo tu. Yaani wanachukulia vitu kirahisi mno tofauti na hali ya mambo ilivyo,"anasema msanii huyo ambaye anaachia singo yake ya 'dakika moja' hivikaribuni.
"Ili kupata mafanikio ya kweli msanii unatakiwa kutoka na kuchanganyika na wenzako kujua nini kinaendelea na wanafanya nini, ndiyo maana unaona mimi napata shoo Rwanda, Kenya, Uganda.
"Niko karibu na watu wengi na kazi zangu zinapigwa sana kule kwavile nimejitangaza kikamilifu na nina mtandao mkubwa kuanzia kwa wasanii mpaka mapromota mbalimbali na hilo siwezi kufanikiwa kama sikujituma.
"Angalia wenzetu wanavyokuja Tanzania kwa kasi kufanya shoo na kukusanya fedha, hii ni kutokana na juhudi zao na ubunifu. Naweza kukwambia katika wasanii wote wa nje wanaokuja hapa ni vigumu kukuta wasanii wetun wa Tanzania wakitaka kujifunza kutoka kwao hata kubadilishana namba au hata njia zozote za mawasiliano ili kesho na keshokutwa wafanye kazi pamoja.
"Namna hii hatuendi tutazidi kubaki hapahapa na hilo si jambo zuri kwa maendeleo ya msanii, unatakiwa kujifunza na kuwa na mtandao mkubwa mimi kazi zangu zinasikika Nigeria kwavile wasanii kama P-Square, J Martin niko karibu nao sana na nimefanya nao kazi.
"Lakini nisingeweza kufika huko kama ningekuwa muoga au nisingekuwa mtu wa kujichanganya na kupenda kujifunza,"anasema msanii huyo wa zamani wa East Coast.